Habari za Punde

RAIS KARIA AIAGA TIMU YA WATOTO WA KITUO CHA WATOTO WENYE MAZINGIRA MAGUMU CHA TANZANIA STREET ACADEMY (TSC)

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF Wallace Karia leo ameiaga timu ya Watoto wa Kituo cha Watoto wenye mazingira magumu kutoka kituo cha Tanzania Street Academy (TSC) cha jijini Mwanza waliokwenda nchini Russia kwenye Kombe la dunia kwa Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.
Timu hiyo imeondoka leo kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar wakiwa na wachezaji 9 na viongozi 4 kutimiza jumla ya watu 13 kwenye msafara wao.
Rais wa TFF Ndugu Karia ameitakia heri katika safari yao hiyo ya Russia akiwataka kufahamu wanabeba bendera ya Tanzania ambayo ina heshima kubwa hivyo wahakikishe wanafanya vizuri.
Amesema TFF inaamini timu hiyo itafanya vizuri kama ilivyokuwa mwaka 2014 waliporudi na kombe kutoka nchini Brazil kwenye mashindano kama hayo.
Naye Rais wa Taasisi hiyo ya TSC Altaf Mansoor ambaye pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Moil ameshukuru ushirikiano mkubwa kutoka kwa TFF ambao wametekeleza kila kilichoombwa pamoja na serikali na sehemu iliyobaki ni kwa vijana hao kwenda kufanya vizuri na kurudi na kikombe.
Katika hatua nyingine Rais wa TFF Ndugu Karia amesema ili kuhakikisha TFF inajikita katika maendeleo ya mpira wa miguu TFF imewaachia Bodi ya Ligi kuwa huru kusimamia Ligi Kuu na Daraja la Kwanza na TFF inaingia pale tu wanapoona mambo hayaendi sawa.
Amesema TFF inasimamia zaidi sera,timu za Taifa na Ligi za chini ikiwemo Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inayoendelea kwenye vituo vinne vya Geita,Rukwa,Singida na Kilimanjaro.
“Uongozi wangu umepunguza mzigo na kuacha huru vitu vingine vifanywe na Bodi ya Ligi kwa kuwaacha huru na sisi tunasimamia sera na timu za Taifa na mafanikio mnayaona na yatakuja mengi zaidi” amesema Karia.
Ameongeza kuwa ni vizuri watu kuwa na mtazamo chanya kuondokana na mtazamo hasi ambao siku zote hukimbiza wadhamini wanaotaka kuingia kwenye mpira wa miguu akiwataka wadau kubadilika katika mtazamo wao kwakuwa hata TFF iliyopo madarakani tayari imebadilika.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.