Habari za Punde

WAOGELEAJI SABA WA TANZANIA WAAHIDI KURUDI NA MEDALI MICHEZO YA DUNIA

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Tanzania Bara (BMT), Mohamed Kiganja (wa sita kulia) akimkabidhi bendera kwa nahodha wa timu ya kuogelea ya Tanzania, Aaron Akwenda (watano kushoto) timu hiyo ambayo itashiriki mashindano ya dunia kwa shule za Kimataifa ambayo yanafanyika Morocco kuanzia leo (Mei 2).
*****************************************
Waogeleaji saba wa Tanzania wametamba kufanya vyema katika mashindano ya dunia ya Shule za Kimataifa (ISF) yaliyopangwa kuanza leo mjini, Marrakesh, Morocco.
Nahodha wa timu hiyo, Aaron Akwenda alisema hayo wakati wa kukabidhiwa bendera jana na serikali. Bendera hiyo ilikabidhiwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT)
Mbali ya Akwenda, waogeleaji wengine ni Shivani Bhatt, Khaleed Ladha, Niamh Baker, Yuki Omori, Dhashrrad Magesvaran na Caleb O’Sullivan.
Waogeleaji wapo chini ya kocha John Belela na viongozi wengine ambao ni Beena Patel, Divyangna Bhatt, Mark Eugene na Lingeswary Ramasamy.
Aaron alisema kuwa wamejiandaa vyema katika mashindano hayo pamoja na wanashiriki kwa mara ya kwanza.
“Tumejiandaa vyema chini ya kocha wetu, Belela, waogeleaji wote wana morali ya hali ya juu kwa ajili ya mashindano hayo, tunatarajia kupata ushindani mkubwa kutoka kwa wanafunzi kutoka nchi nyingine,” alisema Aaron.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja amewaomba waogeleaji hao kufanya vyema na kuiletea nchi sifa.
“Nawaomba mtuletee medali huko Morocco, mimi nilishiriki kuipigania nchi kuingia katika mashindano hayo katika mkutano mkuu uliofanyika Morocco, naomba msituangushe,” alisema Kiganja.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kuogelea nchini (TSA) Inviolata Itatiro alisema kuwa waogeleaji hao wamejiandaa vyema na kuahidi kuleta medali.
“Hatuna wasiwasi na waogeleaji wetu, tunaamini wataleta medali hapa nchini pamoja na kujiandaa kwa kipindi kifupi, mashindano yanatarajiwa kuwa magumu sana kutokana na ukweli kuwa tutashindana na nchi ambazo zimepiga hatua katika mchezo huu,” alisema Inviolata.
“Hatuna wasiwasi na waogeleaji wetu, wamejiandaa vyema na tunaamini kuwa wataleta sifa kwa Taifa na kupromoti mchezo kwa jumla,” alisema Inviolata.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.