Habari za Punde

WATUMISHI WATATU WA HALMASHAURI YA KALIUA MATATANI KWA KUSHINDWA KUONYESHA ZILIPO MILIONI TATU ZA UJENZI WA MADARASANA TIGANYA VINCENT, TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kwa tuhuma za kukiuka taratibu za manunuzi wakati wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Susitila na hivyo kusababisha upotevu wa milioni tatu za nguvu za wananchi. Hatua hiyo ilitokana na taarifa ya Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hiyo kubaini ukiukwaji wa taratibu mbalimbali zilisababisha shilingi milioni tatu kutokuwa na maelezo juu ya matumizi yake.
Alisema jengo hilo ambalo bado halijakamilika linaoonyesha kutumia milioni 6 ambazo hazilinganisha na hali halisi lilipofikia jengo wakati katika shule za jirani ya Imalampaka imetumia milioni mbili kujenga vyumba viwili vya madarasa hadi kufikia hatua ya kuezekwa. Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kaliua kuhakikisha anawachukulia hatua ikiwemo kurudisha shilingi milioni tatu ambazo hazionekana matumizi yake, kushushwa vyeo na kuondolewa katika nafasi zao kwa wale ambao watabainika kutenda kosa.
Alisema hatua isipochukuliwa inawakatisha tamaa wananchi ambao wanajitolea nguvu zao katika kuchangia miradi ya maendeleo huku fedha zikiishia mifukoni mwa wachache. Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dkt. John Pima akitoa taarifa ya ukaguzi maalumu alisema Mkaguzi amebaini ukiukaji wa Sheria, taratibu, kanuni na utoaji wa taarifa za uongo kwa viongozi na umma.
Alisema Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Mtakuja Josephine Benjamin alishindwa kutimiza wajibu na hivyo kutozingatia sheria, taratibu na kanuni wakati wa ukusanyaji na matumizi ya fedha zilizotokana na michango ya wananchi.
Dkt. Pima alisema kwa upande naye Kaimu Mkuu wa Shule ya Susitila Juma Kitwama alitoa taarifa za uongo kwa Mkuu wa Mkoa na umma kwa kutoa taarifa ambayo hakuwa na uhakika nayo juu matumizi ya milioni sita zilizotokana na michango ya wananchi.
Dkt. Pima aliongeza mtuhumiwa huyo pia alishindwa kutoa viambatanisho vinavyothibitisha matumizi ya fedha hizo na kusema kuwa hana viambatisho vya matumizi ya fedha hizo kwa kuwa alipewa taarifa hiyo kutoka kwa aliyekuwa Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Susutila Mussa Elias.
Mapema wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Wilaya mbalimbali alisimamisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa baada ya kutoridhishwa na taarifa ya matumizi ya fedha katika mradi huo na kuagiza Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri kupitia na kisha kutoa taarifa kwake.
Alichukua uamuzi huo ikiwa ni sehemu ya kutaka kuzuia ubadhirifu ambao ungeweza kutokana na fedha nyingine milioni 24 walizopatiwa na Serikali kupitia Equip T ili kukamilisha mradi huo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.