Habari za Punde

JKCI KUSHIRIKIANA NA UBALOZI WA MAREKANI NCHINI TANZANIA KUJENGA TANZANIA YENYE AFYA BORA YA MOYO

Mkurugenzi wa Magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akielezea maendeleo ya ukarabati wa jengo la watoto kwa Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson (wa pili kulia) alipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Marekani (Madaktari Afrika).
Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson akitoka kuangalia ukarabati wa jengo la watoto la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Marekani (Madaktari Afrika).
Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson akiongea jambo na madaktari kutoka Marekani (Madaktari Afrika) walioko katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kambi maalum ya matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo. Jumla ya wagonjwa nane wameshafanyiwa matibabu katika kambi hiyo na hali zao zinaendelea vizuri.
Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson akimsalimia mtoto Catherine Mapunda ambaye amefanyiwa upasuaji wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mhe. Patterson alitembelea Taasisi hiyo leo kwaajili ya kuona kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wataalam kutoka nchini Marekani (Madaktari Afrika).
Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson (wa tatu kulia) pamoja na msafara wake wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kumaliza ziara yake ya kutembelea kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wataalam kutoka nchini Marekani (Madaktari Afrika)
Naibu Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Inmi Patterson akisalimiana na viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili kutembelea kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wataalam kutoka nchini Marekani (Madaktari Afrika). Picha na JKCI
*************************************************
Na Genofeva Matemu na Salome Majaliwa 
14/8/2018 Ubalozi wa Marekani nchini umeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika utoaji wa huduma bora za matibabu ya moyo kwa wananchi. 
Ahadi hiyo imetolewa leo na Naibu Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Dkt. Inmi Patterson alipotembelea kambi maalum ya matibabu kwa wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo inayofanywa na madaktari wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Marekani (Madaktari Afrika). 
Dkt. Patterson alisema huduma zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni za muhimu kwani bila kuwa na afya bora maendeleo hayawezi kupatikana, hivyo basi taasisi hiyo ina wajibu wa kuboresha na kuendeleza maendeleo ya nchi kwa kuwafanya wananchi wake kuwa na afya njema ya moyo. 
“Lengo moja wapo la Taasisi hii liwe ni kuboresha afya za watanzania wenye magonjwa ya moyo hususani watoto wadogo ambao mara nyingi wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa hayo katika umri mdogo na kupelekea wengi wao kudhoofika kiafya na kiakili”, alisema Dkt. Patterson. 
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Agnes Kuhenga alisema wataalam walionao wamekuwa wakitoa matibabu bingwa ya moyo huku wakiwa na ndoto ya kuifanya Taasisi hiyo kuwa ya kimataifa kwa kutoa huduma bora na za uhakika kwa wagonjwa wa moyo. 
“Kabla ya kuanzishwa kwa Taasisi hii mwaka 2015 wagonjwa wengi wenye matatizo ya moyo walikuwa wanatibiwa nje ya nchi, hivi sasa wagonjwa wa moyo wanatibiwa hapa nchini kwa kuwa tuna wataalam na vifaa vya kisasa vya kutosha. Tutaendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wa moyo watanzania na ambao siyo watanzania”, alisisitiza Kuhenga. 
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete imekuwa ikishirikiana na madaktari kutoka nchi mbalimbali Duniani zikiwemo za India, Australia, Marekani, Ujerumani, Israel, Falme za Kiarabu na Uingereza kwa kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo hii ikiwa ni njia mojawapo ya kubadilishana uzoefu wa kazi pamoja na kutoa matibabu kwa wagonjwa yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.