Habari za Punde

VYUO VIKUU VIWE NA BODI ILI KULINDA MASLAHI YA WANAFUNZI NA WAHADHIRI

IMEPENDEKEZWa kuwapo na bodi maalumu ya kuwaongoza wahadhiri wa vyuo vikuu kiutendaji na kinidhamu.
Hoja hiyo imetolewa leo bungeni mjini Dodoma na Mbune wa Manonga, Seif Gulamali, wakati akichangia katika mjadala wa kupitisha muswada wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.  Aidha mjadala huo ulikuwa ni kuhusu uanzishwaji wa bodi ya kitaalamu ya walimu nchini ambayo itakuwa na majukumu ya kuinua viwango vya utaalamu wa walimu kwa lengo la kuwafikisha katika daraja stahili na viwango stahiki kitaaluma ili kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya ualimu.
Gulamali ameunga mkono muswada huo na kuongeza kuwa isiwe kwa walimu pekee bali ilenge kwa wahadhiri pia ambao wana wana umoja wao kama UDOMASA kwa wahadhiri wa Chuo kikuu cha Dodoma na UDASA kwa chuo kikuu cha Dar es saalam.
Ameeleza kuwa vyuo vyenye umoja huo lazima kuwe na bodi moja ambayo itawaongoza na majukumu ya bodi iwe ni pamoja na kusajili wataalamu hao kwa ngazi za shahada, uzamili na uzamivu na kujua idadi yao ili kuweza kuwa na takwimu sahihi za idadi ya wataalamu hao.
Pia ameshauri kuwa bodi hiyo iwe na kazi ya kutambua uwezo wao kitaalama sambamba na kusimamia nidhamu hasa malalamiko ya wanafunzi hasa wakike juu ya wahadhiri kwa manyanyaso ya kijinsia.
Aidha amesema kuwa bodi hizo zitakuwa na maslahi kwa pande zote mbili wawezeshaji na wawezeshwaji katika elimu ili kuweza kuzalisha wataalamu wengi na bora zaidi.
Muswada huo uliopita Bungeni utawalenga walimu katika ngazi zote waliohitimu katika vyuo vinavyotambulika kwa ngazi ya Shahada, stashahada na astashahada na utashirikisha taasisi na wizara mbalimbali zikiwemo Utumishi wa Umma, Chama cha Walimu, Maafisa elimu, Wizara ya mambo ya ndani na Ofisi ya Waziri Mkuu.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.